Changamoto ni tele maishani lakini usikate tamaa
MTU asiye na kusudi hukata tamaa haraka, mtu mwenye roho ndogo hukata tamaa upesi. Kukata tamaa ni kutokuwa na roho ya shukrani, ni kuwa mbinafsi. Kukata tamaa ni kutomwamini Mungu; anajua changamoto unazopitia, lakini bado anasema hutajaribiwa kuliko uwezo wako. Liwe liwalo usikate tamaa! Katika Luka 18, Yesu aliwaambia wanafunzi wake wamwombe Mungu kila wakati wala wasikate tamaa.
Aliwapa mfano wa kadhi asiyemcha Mungu wala kujali wanadamu, lakini mwanamke mjane alimwendea akitaka atendewe haki. Ingawaje yule kadhi alikuwa katili alilazimika kumtendea mjane aliyotaka ili asiendelee kumsumbua. Huyu mwanamke mjane alijua alichotaka, aliishi maisha yenye kusudi, alijua hatima yake ilitegemea maamuzi yake, na hakuwa tayari kukata tamaa hadi apate haki yake. Pigania haki yako kwa nguvu zako zote hata kama itakugharimu pumzi yako ya mwisho. Martin Luther King Jr. alisema, "Ikiwa mtu hajapata kitu anachostahili kufia, hafai kuishi."
Usikate tamaa maana Mungu amekutoa mbali, na ni mwaminifu kukufikisha uendako. Kumbuka alikokutoa na upate sababu ya kuendelea, kumbuka alivyokuepusha na maovu mengi maishani. Haupo salama kwa sababu wewe ni mwangalifu sana bali ni kwa rehema za Mungu. Usikate tamaa maana Mungu anakusudia kukupeleka mbali. Bado hajamalizana nawe.
Methali 23:18 inasema, “Maana bila shaka iko thawabu; na tumaini lako halitabatilika.” Usikate tamaa maana una kusudi la Mungu unalohitaji kutimiza maishani. Anakusudi kwa maisha ya kila mtu. Alimzungumuzia nabii Yeremia kuhusu kusudi lake katika Yeremia 1:5, “Kabla sijakuumba katika tumbo la mama yako nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”
Usikate tamaa maana kuna watu wanakutegemea. Ukianguka, wataanguka; ukifaulu watafaulu. Katika 2 Timotheo 2:2,3 Paulo aliandika, “Mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha wengine. Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.” Usikate tamaa maana kuna mahasidi wanaosubiri tu ukate tamaa ili wafurahie. Waaibishwe, wafedheheshwe wanaoifurahia hali yako mbaya. Wavikwe aibu na fedheha wanaojikuza juu yangu (Zaburi 35:26).

No comments:
Post a Comment