Monday, March 31, 2025

Jisemee mema

 Jisemee mema, wewe ni nabii wa hatima yako

CHOCHOTE unachozungumza kujihusu hutimia. Biblia katika Methali 18:21 inasema, “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.” Kila neno linalotoka kinywani mwako lina uwezo wa kukujenga au kukubomoa.

Chagua kwa makini maana wewe ni nabii wa hatima yako. Kuna mchungaji alienda kumwona mgonjwa hospitalini. Ijapokuwa aliona afya ya yule mgonjwa imeimarika sana, alipomuuliza anavyoendelea, yule mgonjwa alisema haendelei vyema.

Daktari alipoingia alimwambia yule mchungaji anamshukuru Mungu maana mgonjwa anaendelea vyema na hivi karibuni atatoka hospitalini. Lakini yule bwana alikataa na kusema madaktari ni waongo, wanasema mambo hayapo.

Watu wote waliomtembelea hospitalini walishuhudia kuwa anaendelea vyema. Lakini alipingana nao akisema anajua anaishi siku za mwisho na ameambiwa wagonjwa wengi wamefilia kwenye kitanda alichokilalia hospitalini.

Ingawaje alishuhudia kuwa hasikii uchungu mwilini, hakuamini atatoka pale akiwa hai. Baada ya siku chache alifariki. Alikuwa nabii mwenye mtazamo hasi.

Maishani kuna majira ya mambo magumu. Kuna wakati unaweza kupitia mambo mazito hadi unashuku uwepo wa Mungu.



Kuna wakati unaodhani ni marafiki wanabadilika kuwa kama wanyama. Kuna wakati unadhani mazingira ni magumu na hayakupi matumaini. Lakini hata ukiwa katika hali hiyo, unaweza kuchagua kuwa nabii wa mambo mema juu ya maisha yako. John Maxwell alisema, “Unaweza kushindwa kubadilisha mazingira yako, lakini unaweza kubadilisha mtazamo wako.” 

Endelea kujinenea maneno mazuri hata kama huoni matokeo mazuri, usikate tamaa. Maneno yako yaambatane na matarajio yako maana umeumbwa kwa mfano wa Mungu na una uwezo wa kuumba.

Hata wengine wakizungumza mabaya kukuhusu, wewe zungumza mema. Maneno yako yanajenga hatima yako. Kama vile wajenzi huwekelea tofali baada ya tofali, jiwe baada ya jiwe, kwa subira hadi nyumba ikamilike, nawe jenga kwa subira, jenga kwa ustadi, kuwa makini hadi ufikie matarajio yako.

Unahitaji mawe machache na muda mchache kujenga nyumba ndogo, lakini utahitaji mawe mengi na muda mrefu kujenga jumba kubwa. Usiwe na haraka, usishindane na mtu yeyote, hujui wanachojenga.

No comments:

Post a Comment

New Life Convention

Every 2nd week of August is set apart for the New Life annual Convention.